Jumapili 9 Novemba 2025 - 10:50
Kutambua Ukweli wa Kihistoria Kuhusu Uongozi wa Ahlul-Bayt (a.s) Lazima Kuambatane na Subira, Hekima na Uvumilivu

Hawza/ Hafla ya maombolezo ya kumbukumbu ya siku ya kupata shahada Bibi Fatimah Zahra (a.s) ilifanyika mjini Abuja ikiongozwa na hotuba ya Sayyid Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Katika hafla hiyo, alisisitiza umuhimu wa kutambua ukweli wa kihistoria wa dhulma waliyofanyiwa Ahlul-Bayt (a.s) na akasisitiza juu ya subira, uvumilivu na hekima katika kufafanua matukio hayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, jioni ya Jumatano tarehe 14 Jamadi al-Awwal 1447 H.Q. (sawa na tarehe 5 Novemba 2025), hafla ya maombolezo ya kumbukumbu ya siku ya kupata shahada Bibi Fatimah Zahra (a.s) ilifanyika kwa kuhudhuriwa na kundi la wanazuoni, wanafunzi wa dini na wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s) kutoka maeneo mbalimbali ya Nigeria, chini ya uongozi na hotuba ya kiongozi wa harakati hiyo, Sayyid Ibrahim Zakzaky (h.), katika makazi yake mjini Abuja.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ibrahim Zakzaky, mwanzoni mwa hotuba yake, aliwapa pole waliokuwepo na kusema: “Kwanza nawapa pole kwa msiba wa Mtume wa rehema (s.a.w.w.) na yale yaliyotokea baada ya kufariki kwake. Baada ya kifo cha Mtume na matukio mengi, hatimaye ilitokea shahada ya bibi wa wanawake wa ulimwengu wote (a.s).”

Alielezea shahada ya Bibi Zahra (a.s) na matukio yaliyopelekea kufariki kwake kuwa ni msiba mkubwa ulioathiri jamii kwa upana, hasa wafuasi wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w.), na akaongeza: “Watu wengi hawajui undani wa msiba huu, na baadhi hata wanakanusha kutokea kwake; jamii kwa sababu ya ujinga haimjui yeye, na hili lenyewe ni msiba mkubwa.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zakzaky aliendelea kumsifu Bibi Fatimah Zahra (a.s) na, akirejea hadithi ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) aliyosema: ‘Yeye ndiye bibi wa wanawake wa Peponi’, alisisitiza kuwa yeye ni bora kuliko wanawake wote waumini.

Alibainisha tofauti zilizopo katika simulizi za kihistoria kuhusu muda wa shahada ya Bibi Zahra (a.s) kuwa zinatokana na utofauti wa vyanzo vya kale, na akaeleza: “Katika maandiko ya kihistoria, zimetajwa siku 75 au 95 kati ya kufariki kwa Mtume (s.a.w.w.) na shahada ya Bibi Zahra (a.s), na hilo ndilo lililosababisha kuwepo vipindi viwili vya maombolezo katika miezi ya Jamadi al-Awwal na Jamadi al-Thani.”

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kisha akarejelea dhulma zilizofanywa dhidi ya Bibi Zahra (a.s) na kusema: “Wale waliomdhulumu walidhihirisha nia zao, na lengo lao lilikuwa kulinda mamlaka yao. Ni jambo la kushangaza kuona leo watu wengine wanatafuta visingizio kwa matendo hayo; inawezekanaje kutoa udhuru mbele ya ukweli ulio wazi kama mchana?”

Akataja kwa undani matukio yaliyotokea baada ya kufariki kwa Mtume, kama vile uvamizi wa nyumba ya Bibi Zahra (a.s), kuchomwa kwa mlango, kuvunjwa mbavu, kupigwa hadi mimba yake ikaharibika, na pia kukamatwa kwa Amirul-Mu’minin (a.s) kwa kisingizio cha kulazimishwa kiapo cha utii kwa khalifa.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zakzaky alisisitiza: “Iwapo ukweli utachunguzwa kwa makini, itabainika wazi kwamba mambo haya hayakuzushwa na Waislamu wa Shia. Wale wanaouliza kwamba vipi jambo hili liliweza kutokea mbele ya Imam Ali (a.s) wanapaswa kujua kuwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa amemuelezea Imam mustakabali wake na kumpa wasia wa kusubiri ili hoja iwe kamili juu ya watu.”

Akaongeza: “Mtume alimuusia Ali (a.s) awe na subira mbele ya matukio; na subira hii haikuwa kwa sababu ya udhaifu, bali ilikuwa ni jukumu la kimungu. Kwa hivyo haiwezi kusemwa kuwa Imam alikengeuka wasia wa Mtume.”

Zakzaky aliendelea kueleza kuhusu namna ya kuswaliwa Swala ya jeneza kwa Bibi Zahra (a.s) na kusema: “Kwa mujibu wa wasia wake kwa Amirul-Mu’minin (a.s), swala yake ya jeneza ilisaliwa usiku kwa siri pamoja na maziko yake. Ali (a.s), akiwa na watu sita, jumla ya watu saba, walimswalia.”

Alinukuu riwaya zinazoashiria kushuka kwa baraka na mvua kutokana na tawasali kwa wale waliokuwa pamoja naye, na akasema: “Kila mara panapotolewa tawasali kwao, rehema za Mwenyezi Mungu hushuka.”

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, akizungumzia kuhusu kufichwa kwa kaburi la Bibi Zahra (a.s), alisema waziwazi: “Mahali pa kaburi lake lilifichwa kwa kuchelea dharau za maadui, kwani baadhi walitaka kulipata kaburi hilo ili waswali juu yake, na Imam Ali (a.s) alinyanyua upanga kuzuia kitendo hicho. Mpaka leo, mahali halisi pa kaburi halijulikani kwa watu, na ni mwanawe tu, Imam Mahdi (a.f.), anayeweza kufichua mahali alipozikwa mama yake.”

Akijibu wale wanaoona historia kama jambo lililopita na lisilo na umuhimu, alisema: “Tukisema ni historia na tuiache ipite, basi itamaanisha hata dini nayo imekuwa historia. Kwa kuwa dini iliharibiwa na watu hao, basi matukio ya kale bila shaka yana athari juu ya dini.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zakzaky alizungumzia umuhimu wa kukabiliana kwa uaminifu na ukweli, kuepuka kuficha au kusababisha fitna, na akasisitiza kuwa watu wanapaswa kuongozwa kuelekea kwenye ukweli kwa akili na busara, si kwa mabishano na ukali.

Aliwasisitizia wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) kwamba: kwa mujibu wa wasia wa Amirul-Mu’minin (a.s) na kwa kuzingatia kiwango cha uelewa wa wasikilizaji, wazungumze kwa uvumilivu na subira, waepuke kutumia maneno makali au lugha ya matusi, kwani mtazamo wa namna hiyo husababisha ujumbe kutoathiri wala kuzaa matokeo, na hata kupelekea upotovu. Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alikuwa akifikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa namna iliyoendana na uelewa wa makundi mbalimbali ya watu.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alitoa wito wa kuwa na ustadi na busara katika kufikisha habari kuhusu dhulma iliyowapata Ahlul-Bayt (a.s), ili watu wapate kufikia ukweli kwa utulivu, na kuepukwe mitazamo ya uchochezi na inayosababisha mgawanyiko.

Pia aliviomba vituo vya utafiti na taasisi za kidini zichunguze malalamiko na sintofahamu za kihistoria, na zifichue ukweli, ili watu wawe imara juu ya msingi wa dini sahihi na maarifa ya kweli.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zakzaky, akizungumzia masomo tunayojifunza kutokana na maadhimisho ya misiba ya Ahlul-Bayt (a.s), alisema: “Hafla hizi zinatufundisha kuhuisha mwenendo wao, kuongeza mapenzi kwao, kujifunza subira na uthabiti, na kutuhamasisha kujitolea kwa ajili ya ukweli.”

Alionya kuwa baadhi ya watu huenda wakajionesha kwa sura ya wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s) lakini kwa vitendo wakawa wanatafuta manufaa binafsi au kutumia vibaya jina lao, kisha akaomba dua akisema:

“Mwenyezi Mungu atuweke miongoni mwa wapenzi wa kweli wa Ahlul-Bayt (a.s), si miongoni mwa wale wanaonufaika kwa jina lao.”

Kisha alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia neema ya kuutambua Uislamu wa kweli na kuifahamu turathi ya Mtume (s.a.w.w.), na akatarajia kuwa ukweli huo, licha ya juhudi za kuuficha kwa ajili ya kulinda mamlaka ya baadhi ya watu, hatimaye utawekwa bayana.

Mwishoni, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Zakzaky aliomba dua akasema:

“Namwomba Mwenyezi Mungu atulinde na shari ya wale wanaotumia jina la kulinda Wakristo kujihusisha na mauaji na ukatili. Ewe Mungu, uitukuze Dini ya Uislamu na udhalilishe ukafiri; wafanye waumini wawe thabiti katika kutekeleza wajibu wao na katika kuwaita watu kwenye dini, na uukaribishe ujio wa Mrekebishaji ambaye kwa kupitia kwake matatizo yote yatatatuliwa.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha